MAISHA ya kijana wa Kitanzania, Clifford Mangula, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yapo katika hatua za mwisho baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki kwenye mauaji ya kinyama ya wasichana sita waliokuwa na vidoa vya urembo kwenye miili yao, yaliyotokea kwenye Tamasha la Campus Night, Novemba 11, 2011.
Baada ya uchunguzi wa kina kufanyika, alama za vidole vya Clifford zinakutwa kwenye moja kati ya miili iliyokutwa ndani ya Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam, mahali mauaji hayo yalipotokea. Alama hizo zinatumika kama ushahidi ambao unamuweka hatiani Clifford ambaye anaenda kukamatwa nchini Canada, akiwa kwenye sherehe ya ndoa yake.
Baada ya kukamatwa, anasafirishwa mpaka Tanzania ambapo taratibu za kesi yake zinaharakishwa kutokana na shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi ambao wanataka muuaji anyongwe hadharani. Anasafirishwa kuelekea Dodoma kwenye kituo cha kunyongea kilichopo kwenye Gereza la Isanga lakini ajali mbaya inaukumba msafara uliokuwa unamsindikiza. Watu wote wanakufa isipokuwa mtu mmoja tu, Clifford.
Licha ya kunusurika kufa kwenye ajali, baada ya kutibiwa na kupata ahueni, adhabu ya kifo bado inamsubiri, na kwa mara nyingine anasafirishwa kuelekea Dodoma, safari hii kwa kutumia helikopta za kijeshi. Anafikishwa mpaka kwenye Gereza la Isanga ambapo bila kupoteza muda anapelekwa kwenye chumba cha kunyongea ambapo anavalishwa kitanzi na kusimamishwa juu ya stuli.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO...
Wakati akijiandaa kutegua stuli ili Clifford aanze kuning’inia, Mkuu wa Gereza la Isanga, Festus Bihawana alipokea taarifa iliyotumwa kwake kwa simu ya upepo ambayo ilimtaarifu kuwa anatakiwa kulichelewesha zoezi la kumnyonga Clifford kwa dakika kadhaa kwani kuna taarifa mpya zilikuwa zimelifikia jeshi la polisi, makao makuu.
“Kikosi namba 7 cha unyongaji Isanga, KUI 7, makao makuu ya polisi hapa. Mmefikia wapi na huyo mtuhumiwa? Kwani tayari mmeshamnyonga?... Over!”
“Hapana afande, ndiyo tupo kwenye hatua za mwisho, kwani kuna tatizo?... Over!”
“Hebu sitisheni kwanza hilo zoezi kwa sababu kuna taarifa mpya zimetufikia hapa makao makuu… Over!”
“Taarifa gani tena afande, turuhusuni tumalize kazi, lisije kutokea lolote akatuzidi maarifa huyu kijana, si unajua ni muuaji hatari sana?...Over!”
“Fuata maelekezo niliyokupa, sitisha zoezi la kumnyonga kwa dakika kadhaa mpaka tupate uthibitisho wa habari hii iliyotufikia. Over and Out!”
Mkuu wa kitengo cha upelelezi alikuwa akizungumza na mkuu wa gereza la Isanga, Bihawana kwa kutumia simu za upepo. Baada ya taarifa ile, ilibidi Clifford asinyongwe kwanza, akaambiwa anatakiwa kuendelea kusubiri palepale huku kitanzi kikiwa kimeshakazwa shingoni.
Clifford, akiwa amesimamishwa juu ya stuli na kuvalishwa kitanzi, aliendelea kumuomba Mungu wake amnusuru kwani aliamini ni yeye peke ndiye anayeweza kumuokoa kutoka kwenye shimo la mauti lililokuwa linamsubiri. Alisimama vile kwa muda mrefu mpaka mwili wake ukaanza kuishiwa nguvu.
Kwa muda wote huo, askari magereza wenye silaha walikuwa wamemzunguka wakati mkuu wa gereza alikuwa ametoka na kuelekea ofisini kwake kwa lengo la kutaka kufuatilia kwa kina kilichotokea Dar es Salaam mpaka kusababisha zoezi lile kusitishwa kwa muda.
“Kuna mabinti wamepatikana katika mazingira ya kutatanisha na wanaeleza kuwa nao walitekwa usiku wa tamasha kubwa la Campus Night, wanatoa ushuhuda hapa makao makuu ya polisi juu ya kilichowatokea lakini cha ajabu, wote wanaeleza kitu kinachofanana.”
“Wapo katika hali gani? Wanaeleza kuwa walikuwa wapi na nini kilichowasibu?”
“Ni habari ya aina yake, wanaeleza kuwa walipotekwa katika mazingira ya kutatanisha wakiwa kwenye tamasha la Night Campus, wasichana hao sita walipelekwa mahali wasipopatambua ambapo walitumikishwa sana kingono na kuteswa, kisha kukatwa vidoa vya urembo kwenye nyuso zao na kutelekezwa kwenye pori kubwa la Magitunda, nje kabisa ya Mji wa Bagamoyo.
“Watu waliowaokota siku mbili zilizopita, wanaeleza kuwa waliwakuta wakiwa hawajitambui kutokana na majeraha makubwa waliyonayo kwenye miili yao na njaa kali waliyokuwa wanaihisi. Walipowaokota walitoa taarifa polisi ambapo walienda kuwachukua na kuwakimbiza hospitali ambapo baada ya huduma ya kwanza, ni mmoja tu ndiye aliyepata nafuu na kuweza kuongea kilichowatokea.
Binti huyo aliyejitambulisha kuwa anaitwa Jokate ndiye aliyetufumbua macho na hivi tunavyoongea na wewe, anaendelea kutoa ushuhuda.
Hebu sikiliza mwenyewe:
“Walitupeleka mpaka kwenye pori kubwa, walipotushusha kwenye gari wakatupeleka kwenye mahandaki makubwa ndani ya pori hilo, baadaye wakaanza kutukata vidoa vya urembo, mmoja baada ya mwingine kisha wakatupiga mihuri pembeni ya vidonda,” alisema Jokate, msichana ambaye alikuwa ni miongoni mwa wenye vidoa vya urembo ambao walipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Maelezo aliyokuwa anayatoa, yaliwashangaza wengi, ikawa kila akizungumza sentensi moja, watu wanaangaliana na kuulizana kama maelezo anayoyatoa ni ya kweli. Kwa kuwa Jokate ndiye pekee aliyekuwa na uwezo wa kujieleza vizuri kuliko wenzake, alieleza kila kitu walichofanyiwa wakiwa wametekwa, ambapo alifichua siri kuwa walikuwa wakinyweshwa dozi kubwa ya madawa ya kulevya karibu kila siku, jambo ambalo liliwafanya muda mwingi wawe wamelala kwenye mashimo.
Yule binti akazidi kueleza kuwa mbali na mateso hayo, waligeuzwa watumwa wa ngono ambapo wanaume wengi walikuwa wakiwaingilia kimwili bila ridhaa yao, tena wakiwa wamelewa kutokana na madawa ya kulevya waliyokuwa wananyweshwa.
Hakuishia hapo, alieleza kuwa watu wote waliokuwa wanawatesa na kuwabaka, walikuwa wakisikika wakitaja jina moja la mwanamke ambaye ndiye waliyekuwa wakimtaja kuwa bosi wao.
Ni maelezo hayo ndiyo yaliyosababisha zoezi la kunyongwa kwa Clifford kusimamishwa kwa muda ili kupisha upelelezi wa kina kutaka kubaini huyo mwanamke ni nani na Clifford anahusika naye vipi.
“Tukimnyonga mtuhumiwa wetu tutakuwa tumekosa nafasi ya kuujua ukweli mpana zaidi. Naamini tukimbana vizuri, atatupa ushirikiano wa kufahamu ukweli uliojificha nyuma ya tukio hili la kusisimua,” alisema mkuu wa kitengo cha upelelezi, Saleh Katera wakati akizungumza na mkuu wa gereza la Isanga, Festus Bihawana.
***
Familia ya mzee Harrison McClaren, baba mzazi wa Anne Marie, mke wa Clifford iliendelea na maombi mfululizo ambapo kwa siku sita, walikuwa wamefunga, wakifanya maombi usiku na mchana. Walikuwa wakisubiri muujiza wa Mungu kumnasua Clifford kutoka kwenye kitanzi.
Licha ya maombi mfululizo, bado hawakuona kama kuna dalili za Clifford kuachiwa. Taarifa ya mwisho ambayo ilimvunja kabisa nguvu Anne Marie, ni pale aliposikia kuwa tayari mumewe alikuwa amevalishwa kitanzi, tayari kwa kunyongwa. Anne Marie aliposikia habari ile, alikimbilia kwenye chumba chake na kujifungia na funguo.
Kitendo cha mumewe kuja kutolewa wakiwa ukumbini kwenye sherehe ya harusi yao nchini Canada, kilimuathiri sana Anne Marie kisaikolojia, akawa haoni tena umuhimu wa yeye kuendelea kuishi duniani. Kama alivyokuwa amejiapiza mbele ya mama yake kuwa mumewe akinyongwa na yeye atajiua, alitaka kutimiza azma yake.
Alifungua begi lake la nguo na kutoa vidonge vingi mchanganyiko alivyokuwa anavitumia kipindi alipokuwa anaumwa. Bila hata kufikiria mara mbilimbili, alichukua karatasi na kalamu na kuandika ujumbe mrefu, akieleza jinsi alivyoumizwa na kitendo cha mumewe kukamatwa na kisha kupelekwa kunyongwa, ikiwa ni saa chache tangu walipofunga ndoa.
Aliandika kuwa ameamua kujiua akiwa kwenye maombi ya siku sita mfululizo ili akifa aende kupumzika peponi, na kama ikiwezekana akutane na mumewe Clifford ambaye tayari alikuwa anaamini kuwa ameshanyongwa. Alipomaliza kuandika ujumbe ule, aliuweka mezani, mahali ambapo aliamini itakuwa rahisi kwa wazazi wake kuuona kisha akachukua glasi ya maji na kuanza kunywa vile vidonge zaidi ya thelathini.
Muda mfupi baadaye, hali yake ilibadilika kabisa, akawa anajinyonganyonga tumbo huku povu jingi likimtoka mdomoni, puani na masikioni. Mwili uliishiwa nguvu na akageuza macho na kuangalia juu.
Je, nini kitafuatia? Usikose wiki ijayo kwenye gazeti hili la Uwazi.
Comment
Comment by Abdallah Mgeleka Dullah on February 27, 2012 at 3:45pm
Comment by Real De' Dear on February 27, 2012 at 1:42pm mh! sasa nahuyu nae duh!
Comment by Daudi on February 23, 2012 at 11:35am Inasisimuaaa........!!!!1
Comment by ANDERSON SOGOLE on February 23, 2012 at 12:04am
Comment by ANDERSON SOGOLE on February 22, 2012 at 11:56pm
Comment by lumi mwandelile on February 22, 2012 at 8:56am mhhhhhhhh
Comment by Ediclad Ansgary Kihinja on February 21, 2012 at 9:22pm Interesting development
| 1 |
GLOBAL |
| 2 |
julius manning |
| 3 |
Man KKK |
| 4 |
Sili Silali |
| 5 |
IL-YA |
| 6 |
chama baby |
| 7 |
msichoke mlugu |
| 8 |
kaka |
| 9 |
Maji Marefu |
| 10 |
Kelvin Luhala Eto'o |
othman Ochu posted a status
mrembo commented on Sili Silali's photo

You need to be a member of Global Publishers to add comments!
Join Global Publishers