Queen of the Gorillas (Malkia wa Masokwe) - 58

BAADA ya kutengana na mkewe, hatimaye Dk Lewis anafanya jitihada za kuiunganisha tena familia yake kufuatia kupatikana kwa mtoto wake wa kipekee, Skyler ambaye alitoweka kipindi kirefu kilichopita.
Dk Lewis na Suzan, wanaenda mahakamani na kula kiapo cha kutengua talaka kisha wanafunga ndoa nyingine ya mkataba, wanarudi nyumbani kwao na kuyaanza maisha mapya ya familia, wakiwa na mtoto wao, Skyler pamoja na mjukuu wao, Harrison.
Siku zinasonga mbele kwa kasi na Harrison anazidi kuwa mkubwa. Anamaliza elimu ya msingi na kuanza shule ya sekondari anakohitimu kidato cha nne. Baadaye anajiunga na chuo cha Michigan State University anakosomea masomo ya tabia za wanyama, Ethology.
Je, nini kitafuatia?
SONGA NAYO...
HARRISON aliendelea na masomo katika chuo cha Michigan State University, School of Ethology. Alipoingia mwaka wa pili, alizidisha juhudi kwenye masomo, jina lake likazidi kupaa miongoni mwa wanachuo na wakufunzi wake kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao kwenye masomo.
Kama ilivyokuwa kwa mwaka wa kwanza, mwaka wa pili ulipoisha Harrison aliongoza kwenye matokeo ya jumla na kushika nafasi ya kwanza miongoni mwa wanafunzi wengi waliokuwa wanasomea Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Zoolojia (Bachelor Degree of Science in Zoology).
Mwaka wa tatu ulipofika, kama ilivyo kawaida kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Marekani, Harrison na wanachuo wenzake walienda kufanya ‘field’. Kwa kuwa Harrison aliamua kubobea katika somo la tabia za wanyama (Ethology), alienda kufanya field kwenye kituo cha kufugia wanyama (zoo) cha Michigan.
“Napenda sana kujua tabia za sokwe na wanyama jamii ya nyani. Nataka kujua kwa nini wanashabihiana na binadamu kwa vitu vingi.”
“Hamna shida, hapa umefika, kuna idadi kubwa ya sokwe, nyani, ngedere na tumbili, naamini utajifunza mengi na nitakuwa sambamba na wewe kukupa msaada wowote utakaoutaka,” alisema Casper Martin, mkurugenzi wa kituo kile cha kufugia wanyama.
Harrison akaanza rasmi masomo yake kwa vitendo, ikawa kila siku anashinda kwenye mabanda ya kufugia wanyama hao huku akirekodi vitu mbalimbali kwa kutumia kamera yake ndogo ya kisasa. Aligundua mambo mengi kuhusu wanyama hao ambayo awali hakuwa akiyajua.
Siku zilizidi kuyoyoma , hatimaye muda wa kumaliza field ukawadia. Harrison akaagana na mwenyeji wake, Casper huku akiahidi kurudi kwenye kituo kile endapo atahitaji msaada wowote. Alirudi chuoni kwao na kuungana na wanachuo wengine kumalizia muhula wa mwisho.
Ripoti ya field ya Harrison alipoiwasilisha mbele ya wanachuo wenzake na wakufunzi, ilionesha kuwa bora kuliko zote zilizowahi kuletwa chuoni pale. Akapata pongezi nyingi kutoka kwa wenzake, na ripoti yake ikatangazwa kushika nafasi ya kwanza, jambo lililozidi kumtia faraja.
“Lazima niwe mtaalam wa hali ya juu wa tabia za wanyama, nitautumia muda wangu mwingi kufanya tafiti nyingi kwa kadiri niwezavyo,” alisema Harrison akionesha kufurahishwa sana na sifa alizokuwa anapewa.
Miezi kadhaa baadaye, Harrison na wenzake walihitimu masomo yao ya chuo, wote wakarudi makwao kusubiri matokeo. Harrison ambaye sasa alishakuwa mtu mzima, alirudi nyumbani kwao, Miami alipokuwa anaishi na mama yake, Skyler, babu na bibi yake.
“Ooh! Hongera sana mwanangu, naamini utakuwa mtu mashuhuri sana duniani kwani matokeo yako ya chuo tangu ulipoanza mwaka wa kwanza ni kielelezo cha uwezo mkubwa uliojaaliwa na Mungu.”
“Ahsante mama, nitakaa hapa nyumbani kwa siku chache tu, nataka wakati naendelea kusubiri majibu nikaendelee na kazi ya utafiti wa wanyama kwenye misitu mbalimbali.”
“Mimi sina pingamizi mwanangu, wewe endelea na kile unachoona kinafaa ila nakuomba utambue kuwa tayari umeshakuwa mkubwa na inabidi uanze maisha ya kujitegemea ili baadaye na wewe uje kuwa na familia yako.”
“Sawa mama, lakini kabla ya yote nahitaji kuifanyia kazi elimu yangu,” Harrison alikuwa akizungumza na mama yake, Skyler mara baada ya kuwasili akitokea chuoni kwao ambapo alihitimu masomo yake.
Pia babu na bibi yake (Dk Lewis na mkewe) walifurahishwa sana na hatua aliyokuwa ameifikia Harrison, kutokana na jinsi alivyokuwa amefanana na baba yake, marehemu Harvey, aliwafanya wasahau machungu yote waliyopitia, ikawa kila siku wanafurahi kumuona.
Baada ya kukaa pale nyumbani kwa muda wa wiki mbili, Harrison aliaga na kuondoka, akachukua vifaa vyote muhimu vilivyokuwa vinahitajika kwa ajili ya safari ya kwenda kufanya utafiti wa tabia za wanyama kwenye misitu mbalimbali nchini Marekani.
Alichukua hema dogo la kuhamishika, laptop, kamera kubwa na ndogo, taa zinazotumia gesi, juisi, maji na vyakula vikavu. Alichukua pia vitabu mbalimbali ambavyo vingemsaidia kwenye utafiti wake.
Akaianza safari ya kuelekea Kaskazini mwa Marekani, kwenye jimbo la Montana kulikokuwa na msitu mnene wa Tongass. Msitu huo uliokuwa na miti iliyofungamana iliyoziba eneo kubwa, ulikuwa ukisifika kwa kuwa na idadi kubwa ya sokwe, nyani, ngedere na wanyama wengine wa jamii hiyo.
Alisafiri kwa kutumia treni ya umeme (metro), safari iliyomchukua zaidi ya saa nane kufika kwenye mji mdogo wa Tongass, mahali kulipokuwa na lango la kuingilia kwenye msitu huo.
Alipofika kwenye ofisi zilizokuwa zinahusika na utunzaji na usimamizi wa msitu huo, Harrison alijitambulisha na kuonesha nyaraka zote muhimu, akaomba kufanya utafiti wa kilichompeleka.
Uongozi wa msitu ule ulimkubalia ila ukampa angalizo kuwa ndani ya msitu ule kuna sokwe wakorofi ambao mara kwa mara wameripotiwa kuwadhuru watalii na watu waliokuwa wakienda kufanya utafiti kama yeye. Akaambiwa ajitahidi kuwa mwangalifu na asiyasogelee makundi ya sokwe hao.
Pia alipewa bastola ndogo iliyokuwa inatumia risasi za mpira kwa ajili ya kujihami inapotokea amekutana na wanyama wakali. Aliushukuru uongozi ule na kuingia ndani ya Msitu wa Tongass. Akaingia mpaka ndanindani kabisa na kutafuta sehemu iliyokuwa na mwinuko, akafyeka vichaka na kuanza kazi ya kuchomeka hema lake.
Aliamua hapo ndiyo pawe makazi yake kwa siku zote atakazokaa ndani ya msitu huo. Alilijenga hema vizuri kiasi cha kufanya hata kama wanyama wakali wakija eneo lile, washindwe kuingia ndani wala kumdhuru.
Alipohakikisha limekaa vizuri, alipanga vitu vyake katika mpangilio nadhifu, akachukua kamera zake mbili, kubwa na ndogo, kijitabu cha kuandikia kumbukumbu (diary) na vitu vingine vidogovidogo, akatoka na kuanza kuyasanifu mandhari ya msitu ule mkubwa.
Kwa kuwa ilikuwa ni siku ya kwanza, hakutaka kwenda mbali, alianza kuchunguza mambo mbalimbali, kuanzia jinsi mimea ya msitu ule ilivyokuwa imefungamana, akawa anapiga picha kwa kutumia kamera zake huku akiandika baadhi ya mambo kwenye kijitabu chake.
Hatimaye giza liliingia, Harrison akarudi ndani ya hema lake na kujifungia, akala biskuti na kunywa juisi kisha akalala. Usingizi haukuja kirahisi kwani kelele za wanyama waliokuwa wakija pale jirani na hema lake na kuondoka zilimfanya muda mwingi akae macho. Baadaye usingizi ulimpitia, akalala mpaka kesho yake alfajiri.
Aliamka alfajiri na mapema, akavaa nguo za kazi na kuchukua vifaa vyake muhimu, akatoka nje ya hema na kuanza kutembea kwenye msitu ule mnene, huku akichunguza mambo mbalimbali na kuyaandika. Akiwa anaendelea kuchunguza mambo mbalimbali, alisikia miti ikitingishika kwa nguvu, kelele za milio ya wanyama zikawa zinasikika kwa nguvu.
Ilibidi akajibanze kwenye mti mkubwa na kuangalia ni wanyama gani, macho yake yakatua kwenye kundi kubwa la sokwe wakubwa waliokuwa wanaruka kutoka tawi moja kwenda jingine kwa kasi kubwa, wakawa wanaelekea pale alipokuwa amejibanza.
Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Views: 1923

Tags: hadithi11

Comment

You need to be a member of Global Publishers to add comments!

Join Global Publishers

Comment by wakusheki mjomba on November 17, 2012 at 10:57pm

nafikri challote akuwa mchumba wa harrison.

Comment by tzzBoy on November 16, 2012 at 3:24pm
Hayo ndio mambo ya wenze2 unasoma kutokana na kipaji ulichonacho. Huyo dogo atakuwa bonge la mtaalam
Comment by de ginnethon jr on November 16, 2012 at 11:57am
dah nahisi ni yule mdada aliye nusulika na ajari ya ndege
Comment by bianca kingu on November 16, 2012 at 11:31am

labda huyo mdada ndio atakuwa mkeo (queen of gorillas)

Comment by FURAHA TAUSI on November 16, 2012 at 11:18am

mmh hiyo kazi siitaki hata kwa dawa

Comment by Emmie Saitoti on November 16, 2012 at 11:18am

haya mtaalamu kazi imeanza ni vyema kuwa makini

 

ADVERTISEMENT


Advertisement

 

Forum

KIPIGO CHA BAO 2-1 KWA MAN UTD, KOSA LA MWAMUZI?

Started by GLOBAL in Burudani. Last reply by Mohammed Mar 26. 6 Replies

JE, NI KWELI KWAMBA KIPIGO CHA BAO 2-1 ILICHOKIPATA MAN UTD KUTOKA KWA REAL MADRID USIKU WA KUAMKIA LEO LAWAMA ZOTE ZIMWENDEE MWAMUZI WA MCHEZO AU MAN UTD WAJILAUMU WENYEWE? TUPE MAONI YAKO!!!

HALI INAYOENDELEA BUNGENI, SPIKA NA NAIBU WAKE WAMESHINDWA KUONGOZA?

Started by GLOBAL in Siasa. Last reply by Ali Abdalla Ali Apr 22. 20 Replies

Tumeshuhudia kwa siku za hivi karibuni hali halisi iliyokuwa inatokea katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Je, kwa hali hii ni ishara kuwa Spika na Naibu wake washindwa kuliongoza bunge hilo?

VURUGU ZA CCM NA CHADEMA KUGOMBEA MLINGOTI WA BENDERA DODOMA, NANI WA KULAUMIWA?

Started by GLOBAL in Siasa. Last reply by Phinehas Rishiansia Kileo May 3. 6 Replies

Wafuasi wa CCM wakimshambulia mfuasi wa Chadema mkoani Dodoma…

Tags: BENDERA, WA, DODOMA, NANI, KULAUMIWA?

VURUGU ZINAZOENDELEA HAPA NCHINI NANI WA KULAUMIWA?

Started by GLOBAL in Siasa. Last reply by NELSON UVAMBE yesterday. 27 Replies

HIVI KARIBUNI KUMEKUWEPO UPOTEVU WA AMANI HAPA NCHINI PAMOJA NA WANANCHI KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI. MKOANI KAGERA WANANCHI WENYE HASIRA WALIWAUA POLISI, IJUMAA ILIYOPITA WAKULIMA NA WAFUGAJI HUKO WILAYANI KILOSA WALIZUA VURUGU NA KUFUNGA BARABARA,…

MRISHO NGASSA KUPELEKWA SIMBA SC BILA RIDHAA YAKE, JE NI HALALI?

Started by GLOBAL in Burudani. Last reply by Domino Bagambisa Jan 21. 17 Replies

Kiungo hatari wa Azam FC, Mrisho Ngassa leo amepelekwa Simba SC kwa mkopo na timu yake…

Tags: SOKA

hivi ni nani yuko sahihi kuhusu uchaguzi wa UMEYA arusha CCM au CHADEMA?

Started by Gysper in Siasa. Last reply by Jamal amor May 9. 24 Replies

 hivi ni nani yuko sahihi kuhusu uchaguzi wa UMEYA arusha CCM au CHADEMA?

Kauli Ya JK kuwa Mauaji ya Arusha ni "Bahati Mbaya"

Started by Kulikoni Ughaibuni in Siasa. Last reply by richardngeze Feb 12. 12 Replies

Tanzania tuna tatizo kubwa.Hakuna haja ya kunyoosheana vidole as to nani amechangia tatizo hilo bali cha muhimu na haraka ni namna tutakavyoweza kutatua tatizo hili.Nisimung'unye maneno: tatizo kubwa linaloikabili ni kuwa na Rais ambaye takriban…

© 2013   Created by Global Publishers.

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service