
Na Mwandishi WetuBado Jiji la Dar limegubikwa na tukio la nyota wa Ligi ya NBA nchini Marekani, Hasheem Thabeet Manka kumkata mtama wa ‘kushiba’ msanii nyota wa Bongo Flava, Khaleed Mohamed ‘TID’, Amani limegundua.
Mbaya zaidi, hali hiyo inakwenda sanjari na utata wa nini hasa kilisababisha tafrani ya nyota hao ambao wanafahamiana vizuri. Gazeti hii lilikwenda mbele zaidi na kusaka ukweli wa pande zote na ifuatayo ndiyo full muvi.
KWA MUJIBU WA SHUHUDA
Anasema ilikuwa mishale ya saa kumi usiku, Ijumaa ya Mei 7, 2010 ndani ya Club Billicanas ambapo msanii wa Bongo Flava, TID aliingia akiwa ameambatana na kimwana.
Akazidi kuweka wazi kuwa, TID na demu huyo walionekana kuzunguka zunguka na kusalimiana na baadhi ya watu lakini muda si mrefu, aliingia Hasheem akiwa ndani ya gari lake la kifahari aina ya Range Rover Sport jeusi lenye namba za usajili T SSS 101.

Hasheem Thabeet
Shuhuda huyo anasema kuwa, nyota huyo akiwa na wapambe wake wawili alikwenda kukaa kaunta na kuanza kuagizia vinywaji, lakini ghafla TID akiwa na kimwana wake walipita jirani na Hasheem, “yule demu akamwita Hasheem, kisha akaenda kumsalimia, lakini TID akaenda mbele na kusimama akiwaangalia,” alisema shuhuda huyo.
Akizidi kuweka wazi tafrani nzima, sosi huyo anasema: “Ghafla TID alisema umemwona huyo tu (yule demu), sisi wengine hukutuona.”
Anaendelea kusema kuwa, Hasheem akiwa amevalia ile kapero yake alimjibu TID kuwa, hakumwona lakini si mbaya akamsalimia mambo vipi?
Shuhuda huyo makini anasema kuwa, TID huenda alikuwa na lake jambo kwani pamoja na salamu hiyo alianza kumtukana jamaa (Hasheem) huku akimwambia maneno ya kejeli, “lakini jamaa alikuwa akimuonya kuacha kumtukana,” alisema.
Akasema baadhi ya watu waliokuwemo ndani walianza kuhisi kitu kwani walisikika wakisema TID anataka kufanya vurugu kutokana na historia yake anapokuwa Club au sehemu mbalimbali za burudani.
Shuhuda huyo anaendelea kusema: “Ukweli Hasheem alimwonya TID karibu mara nne aache kumsemea mbovu, lakini jamaa akaendelea hadi Hasheem akashikwa na hasira na kusimama, TID akasogea mbele lakini huku akiendelea kumtukana jamaa.”

Khaleed Mohamed ‘TID’
Anasema TID alipomwona Hasheem anazidi kumfuata, akakimbilia nje ndipo Hasheem alipomkimbiza hadi huko na kumpiga mtama huku akimuuliza ni kwanini amemtukana bila sababu licha ya kumwonya kuacha kufanya vile.
Sosi anamwaga zaidi kwa kusema kuwa, baadhi ya watu ndani ya ukumbi walisikika wakisema kwa hatua aliyofikia TID, hata angekuwa nani asingeweza kuvumilia maana alimtukana karibia mara kumi.
Akasema: “Tena ana bahati sana, Hasheem kampa nafasi mara nne akimwonya asiendelee kumtusi, lakini hakusikia.”
Inadaiwa zaidi kuwa, wapambe na mabaunsa walimfuata Hasheem na kumvutia pembeni ndipo nyota huyo ambaye yupo Bongo kwa mapumziko, akaamua kuondoka zake akimwacha TID akiugulia maumivu chini.
ANAVYODAI TID MWENYEWE
Baada ya kimbembe hicho, msanii huyo wa Bongo Flava aliamua ‘kumwaga mboga’ akisema kile kilichojiri hadi kujikuta akilimwa mtama na nyota mwenzake huyo.
Anasema: “Ilikuwa saa kumi na nusu nikiwa natoka Club Billcanas na rafiki yangu Anna huku naongea na simu na Hisbert (sijui ni nani?) kwa sauti ya juu maana kelele za muziki zilikuwa zinasumbua, nikiwa nimesimama nje ya mlango wa kioo ghafla akatokea Hasheem ambaye alikuwa ‘Kaunta’ akiongea na wakata tiketi, akanipiga bonge la mtama nikaanguka chini na kuzirai kwa dakika kadhaa.
“Mabaunsa wakanibeba na kuniweka pembeni maana nilikuwa mlangoni, nilipozinduka nilisikia maumivu makali kwenye mabega, mkono wangu wa kulia na mguu ambao unafanya kutembea kwangu kwa taabu, nikaangalia mkononi simu yangu sikuiona, nikawauliza mabaunsa yule jamaa amekwenda wapi, wakadai ameondoka tayari…
“Nikajikokota kuelekea kwenye gari yangu na kuelekea Polisi kutoa taarifa niweze kupata matibabu. Nilipofika nikaandika statement na kupewa namba ya case CD/RB/6848/10 pia nikapatiwa PF3 (Fomu ya Polisi namba 3) nikaenda hospitali kupata matibabu.
“Sasa hivi (Jumanne) niko kitandani siwezi kutembea vizuri, pia nitashindwa kuperfom (kutumbuiza) kwenye harusi ambayo tayari nimeshalipwa pesa.”
SWALI LA TID
“Swali langu ni kwanini ameamua kunidhalilisha vile mbele ya CLUB na FANZ (mashabiki) ambao nilikuwa nawatumbuiza? Kwanini ameamua kuniharibia kazi yangu? Kwanini ameamua kunipiga bila ya kumkosea? Je, ni sawa hivi jamani….naona machozi yananitoka sina cha kumweleza mama yangu.”
ALICHOSEMA HASHEEM
Baada ya maelezo hayo, Amani liliongea na Hasheem Thabeet ambaye kama TID ‘alimwaga mboga’, yeye ‘amemwaga ugali’ ambapo anadai TID ni mchokozi.
Anasema kuwa, siku ya tukio akiwa na kampani yake walikwenda Club Billicanas, wakaingia ndani ‘kujiachia’.
Hasheem anasema: “Tulikwenda kukaa Kaunta na kwa sababu huwa nakunywa kwa kusaini mahali, nilifanya hivyo, mhudumu alinipa kalamu na kitabu cha kusaini.”
Anasema akiwa anamwaga wino, alisikia sauti ya kike ikimwita kwa jina, Hasheem! Akaacha ‘kuanguka kitabuni’ na kuangalia ilikotokea sauti hiyo.
Anasema: “Nilimwona msichana mmoja akiwa ameongozana na TID. Lakini yule msichana alikuja nilipo, akajitambulisha, nikawa najaribu kumkumbuka. Wakati huo TID alikwenda hatua kadhaa mbele na kusimama akituangalia.
“Ghafla akasema nimeona wengine tu, yeye (TID) sikumwona. Nikamjibu ni kweli sikumwona, ila yeye kwa sababu ndiye aliyeingia, alipaswa kunisalimia iwapo aliniona kama alivyofanya yule msichana aliyeongozana naye,” alisema Hasheem.
Akasema, lakini majibu ya Mbongo Flava huyo aliyewahi kufungwa jela kwa kosa la kumpiga mtu, hakuyategemea, kwani alimwambia asijifanye yeye (Hasheem) ni staa sana, hana lolote.
Hasheem anasema alicheka akiamini TID alikuwa akimtania tu, lakini akakasirishwa na staa huyo kumwambia ‘unacheka nini sasa’.
“Niliamua kucheka kwani TID namfahamu siku nyingi, lakini aliponiambia unacheka nini sasa, ndipo nikajua kumbe yupo kishari, nikamwonya kuwa, asiendelee kunisemea mbovu.”
Anasema licha ya kumwonya mara ya kwanza, ya pili na ya tatu, TID aliendelea kusema ‘mbofumbofu’ hali iliyompandisha hasira nyota huyo na kuamua kutoka naye ‘baruti’ mpaka nje ambako alipom’bamba alimpa mtama wa sawasawa, jamaa akaenda ‘dauni’.
Anasema alipoona jamaa hasimami kujibu mapigo, yeye aliamua kutimua zake ‘mahom’ Sinza lakini baadaye alifuatilia na kuambiwa msanii huyo aliamka na kuondoka zake.
SWALI LA HASHEEM
“Ni kwanini TID aliamua kunisemea mbovu huku nikimwonya mara tatu asiendelee kufanya vile? Je, alitaka litokee lililotokea ili tuhadhiriane mbele za watu? Nimesikitika sana, mimi sina historia ya kudundana na watu katika maisha yangu.”
Wakati huo huo, habari zinadai kuwa, mmiliki wa Billicanas, Freeman Mbowe amempiga marufuku TID kuingia kwenye ‘kiwanja’ hicho baada ya kuzidi kuendeleza tafrani usiku huo huku yeye mwenyewe Mbowe akishuhudia.
You need to be a member of Global Publishers to add comments!
Join Global Publishers